Wilaya ya A-C-T imekuwa ya kwanza nchini Australia, kutoa chanjo kamili kwa 95% ya umma wayo wenye miaka 12 na zaidi dhidi ya UVIKO-19. Taarifa hiyo imejiri siku moja baada ya tangazo kuwa 80% wa Australia wote wenye miaka 16 na zaidi wamepokea dozi mbili za chanjo. Jimbo la New South Wales linakaribia kufikisha 90% ya lengo ya chanjo kamili, kwa watu wenye miaka 16 na zaidi, wakati 89.7% ya watu jimboni humo kwa sasa wamepata dozi mbili za chanjo.
Mamia kwa maelfu ya watu wameandamana leo katika miji mbali mbali nchini Ethiopia dhidi ya kundi la wapiganaji la Tigray People's Liberation Front (TPLF) huku serikali kuu ya nchi hiyo ikijipata chini ya shinikizo kufuatia kusonga mbele kwa wapiganaji wa kundi hilo kuelekea mji mkuu, Addis Ababa. Waandamanaji hao walikusanyika kwa amani na kuapa kuliunga mkono jeshi la nchi hiyo dhidi ya kundi hilo la TPLF linalopigania uhuru zaidi katika eneo la Tigray lililoko Kaskazini mwa nchi hiyo.
Mabalozi wa nchi za jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika magharibi ECOWAS wamekutana na Waziri wa mambo ya nje wa Guinea mjini Conarky, kabla ya kufanyika kongamano la jumuiya hiyo litakalofanyika jumapili kujadili hali ya usalama nchini Guinea na Mali. Jumuiya hiyo imesitisha uanachama wa Guinea na kutaka viongozi wa mapinduzi kuachilia huru rais Alpha Conde. Viongozi wa mapinduzi ya kijeshi wametakiwa pia kuandaa uchaguzi mkuu na kurejesha utawala wa kikatiba nchini Guinea.