Victoria imerekodi kesi mpya 37,994 za COVID-19 na vifo 13, wakati virusi hivyo vikiendelea kuathiri huduma za umma pamoja na magari ya wagonjwa (ambulance).
Maambukizi mapya jimboni humo ni pamoja na kesi 18,503 kutoka kwa vipimo vya haraka vya antijeni na 19,491 kutoka kwa vipimo vya PCR, idara ya afya ilisema Jumanne.
Kuna wagonjwa 861 hospitalini, 43 zaidi ya siku iliyopita, ikiwa ni pamoja na 117 wako ICU na 27 wakisaidiwa kupumua kutumia mashine.
Jimbo hilo kwa sasa linapambana kusimamia kesi 171,369.
Takwimu za hivi punde zinakuja huku wahudumu wa afya wa Victoria wakionya kuwa kutakuwa na ucheleweshaji wa ambulensi kuwafikia watu kwa mara ya pili katika wiki.
Ambulance Victoria (AV) ilisema ilikuwa inakabiliwa na "mahitaji makubwa sana ya magari ya wagonjwa" katika jiji kuu la Melbourne.
"Kuna uwezekano kutakuwa na kuchelewa kwa ambulensi kukufikia," ilisema katika taarifa yake leo hii.
"Kipaumbele chetu ni kutoa huduma kwa Wakazi wa Victoria ambao wanahitaji msaada wa kuokoa maisha."
AV iliwataka Wavictoria kutumia namba sifuri mara tatu pekee kwa dharura na kuwasiliana na Nesi Kwenye Simu au kumtembelea daktari wa eneo lao ikiwa ni ugonjwa na sio dharura.